Latest Updates

HUJAFA HUJAUMBIKA...SIO MIMBA NI UGONJWA HUU JAMANI..MATESO ANAYOPATA MAMA HUYU WE YASIKE TU...!





“MWANANGU dunia hii, hujafa hujaumbika. Kama huamini maneno hayo ya wahenga amini kupitia kwangu,” ndivyo alivyoanza kusema Mariam Manyata (57) mwenyeji wa Mkoa wa Manyara ambaye yupo Hospitali ya Taifa Muhimbili akisumbuliwa na tatizo la tumbo kujaa maji.

Mwanamke huyo aliyebahatika kupata watoto watano wa jinsia ya kike, anasumbuliwa na ugonjwa huo kwa miaka mitano sasa huku madaktari wakimwambia pia mirija ya kupitisha maji imeziba.
UGONJWA ULIVYOANZA
Mwanamke huyo alisema kuwa, alianza kuhisi maumivu ya mwili mzima huku macho yakipoteza nguvu ya kuona sawasawa. Kidogokidogo tumbo lake lilianza kuvimba na kuonekana kama mwanamke mwenye mimba.

MATESO ANAYOYAPATA
Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita, mwanamke huyo alisema kutokana na hali hiyo ya tumbo kuvimba akaanza kuishiwa uwezo wa kupumua sawasawa, pia kushindwa kula chakula cha aina yoyote ile.

ALIKUJAJE MUHIMBILI?
Anasimulia kwa uchungu: “Siyo kwamba nililetwa hapa Muhimbili, bali nilipoona hali inazidi kuwa mbaya ikabidi niuze mazao yangu ambapo nilipata fedha ya nauli ya kunifikisha Dar mimi na mabinti zangu wawili.

“Nilipofika hapa Dar nilitafuta nyumba ya kukaa, nikapata Gongo la Mboto. Lengo iwe rahisi kuja hapa hospitali na kurudi. Mwenye nyumba baada ya kuona hali yangu aliniambia niwe nalipa shilingi 10,000 kwa kila mwezi badala ya 30,000 wanayolipa wapangaji wengine.

“Namshukuru kwa huruma yake kwani mimi niko hospitali lakini hapo kwenye nyumba wanakaa watoto wangu wawili ambao wananisaidia.”

ATOLEWA MAJI LITA 6
Mama huyo alisema Jumanne iliyopita akiwa nyumbani alipata maumivu makali sana, akakimbizwa hospitalini hapo ambapo siku mbili mbele madaktari walimtoa maji kiasi cha lita 6 ndani ya tumbo lake.

Anasema: “Lakini pamoja na kutolewa maji hayo mengi bado siku iliyofuata hali ya tumbo kujaa ilikuwa vilevile. Sina ujauzito jamani, ni maji tu yamejaa tumboni mwangu.”

WALICHOMWAMBIA MADAKTARI
Mama huyo, huku akilia aliongeza kusema kwamba, madaktari walimweleza anaweza kupona tatizo lake lakini fedha walizomtajia kununulia vifaa ni kubwa na yeye hana uwezo wa kuzipata.

KITAALAM SASA
Kwa mujibu wa daktari mmoja wa Muhimbili, tatizo la tumbo kujaa maji husababishwa na protini kupungua kwenye damu. Mfano, maini hutengeneza protini lakini pombe huharibu maini kwa hiyo maini yakiharibika protini kwenye damu hupungua na kusababisha maji kutoka kwenye mirija ya damu na kujaa tumboni.
Kwa sasa mama huyo amelazwa kwenye Jengo la Mwaisela Wadi Namba 3. Kwa yeyote aliyeguswa na tatizo lake anaweza kumsaidia fedha kwa kutumia namba yake ya simu 0757 196 872. Simu hii wakati mwingine inapokelewa na binti yake, Zawadi Jackson.