Latest Updates

AL SAEDY KUANZISHA MFUKO WA MTOTO NASRA ALIYEKUWA AMEFUNGIWA KWENYE BOKSI MIAKA 3


Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Alsaed, Omary Al Saed wa mjini Morogoro anakusudia kuwasiliana na wadau wenzake ili kuanzisha Taasisi ya Nasra Mvungi Foundation, ili kuonyesha namna walivyoguswa na mateso na hatimaye kifo cha mtoto huyo aliyefichwa kwenye boksi kwa muda wa miaka mitatu.



Mtoto huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni mosi mwaka huu, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam alikokuwa amelezwa kwa matibabu ya nemonia.


Nasra ambaye kifo chake kimewagusa watu wengi ndani na nje ya Mkoa wa Morogoro, alizikwa juzi katika makaburi ya Kola mjini hapa.


Akizungumza na gazeti hilo jana, Al Saed alisema amehuzunishwa na mateso na hatimaye kifo cha mtoto huyo na kwamba, ili kuonyesha kuwa ameguswa, ameamua kuwasiliana na wadau wengine ili waone uwezekano wa kuanzisha mfuko huo.


Alisema mfuko huo pia utatumika kuwasaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na wenye mahitaji muhimu.

Alisema hiyo ni njia nzuri ya kukumbuka kifo cha mtoto Nasrah na maisha aliyoishi wakati wa uhai wake.


Mkurugenzi huyo pia alisema atajenga kaburi la mtoto huyo ili iwe kumbukumbu ya kudumu kwa watu wa familia yake na jamii kwa ujumla.


Alsaed alisema ujenzi wa kaburi hilo utafanyika mwishoni mwa wiki hii kwa kutumia marumaru.


Wakati huo huo, Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali mkoani Morogoro, Sunday Hyera amesema hajui chochote kuhusu namna kesi inayowakabili watu wanaotuhumiwa kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo itakavyo kuwa.


Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mariamu Said ambaye ni mama mkubwa wa Nasrah, baba yake mzazi Rashidi Mvungi na mume wa Mariamu, Omary Mtonga.


Chanzo: Mwananchi.