Mtuhumiwa wa wizi wa ng'ombe akiwa kwenye majani yaliyotumika kumchochea moto mara baada ya kupata mkong'oto wa nguvu kutoka kwa wamiliki wa ng'ombe hao huko Mwasanga, Ivumwe jijini Mbeya.
MTU mmoja anayetuhumiwa kwa wizi wa ng’ombe na ndama wake, mwishoni mwa wiki iliyopita alipata kipigo cha kufa mtu na baadaye kuchomwa moto, lakini katika hali isiyo ya kawaida, hakuweza kufariki ‘kugoma kufa’ hadi polisi walipotokea na kunusuru maisha yake.
tukio hilo lilitokea Mwasanga, Ivumwe jijini Mbeya kufuatia kuibiwa kwa wanyama hao usiku nyumbani kwa Kongoro Mwakitalima, ambaye ni mkazi wa Isyesye Kata ya Ilomba.
Ilidaiwa baada ya mwizi huyo kuwachukua wanyama hao, mtu huyo aliwapa taarifa majirani zake, ambao asubuhi na mapema walijihimu na kuanza kuwatafuta ambapo baada ya kufika eneo la Ivumwe walikutana na mwendesha bodaboda ambaye aliwaambia alikutana na mtu akiwa anaswaga mifugo hiyo.
Walipoambiwa hivyo, wananchi hao wakitumia bodaboda, walimfukuzia mtu huyo na kufanikiwa kumkuta katika eneo la Mwasanga relini akiwa na ng’ombe hao.
Shuhuda alisema wananchi walikusanyika na kuanza kumshushia kipigo kikali, lakini licha ya uzito wa mkong’oto, bado mtuhumiwa huyo alionekana kuwa ngangari ndipo waliamua kumchoma moto.
Hata hivyo, licha ya moto huo, bado mtu huyo hakuweza kukata roho hadi askari polisi walipofika eneo hilo na kumchukua.
Hadi tunaingia mtamboni hakuna taarifa zilizothibitisha kama mtuhumiwa huyo alikuwa hai au la!