Latest Updates

USAFIRI: Sumatra yaiamuru Uda kushusha nauli


Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imetoa amri kwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam kutoza viwango sawa vya nauli kama vinavyotozwa na daladala za kawaida.

Sumatra imetaka punguzo hilo la viwango vya nauli kwenda sanjari na mabadiliko na tiketi za mabasi ya Uda ikielekeza zianze kutumiwa wiki ijayo, huku Uda ikikiri kupokea agizo na kuahidi kulitekeleza.

Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki wa Sumatra, Conrad Shiyo alisema kuwa, kumekuwa na usumbufu kwa abiria hasa wanaoutumia usafiri wa Uda, huku makondakta wake wakitoza

viwango vya juu vya nauli na kukatisha ruti kinyume na taratibu akibainisha suluhu ni kufanya mabadiliko hayo.

“Tumeshapeleka mapendekekezo ya mchoro wa tiketi mpya na viwango vya gharama za nauli makao makuu, hivyo tunasubiri marejesho kutoka kwao ili utekelezaji uanze.Mchoro huo unaonyesha ruti ya gari pamoja na kiwango cha nauli abiria anachotakiwa kulipa,”alisema Shiyo na kuongeza:

“Nauli kwa ruti za mjini ambazo siyo za safari za mbali kwa maana ya umbali wa kilomita 14 zitagharimu Sh400 hadi 450. Kwa ruti zinazoanzia kilomita 15 hadi 25 nauli yake itakuwa Sh750…hivyo ndivyo viwango vipya vya nauli za mabasi ya Uda zinazopaswa kuanza kutumika wiki ijayo.”

Alisema, katika kuhakikisha hilo linakuwa endelevu na wananchi wanaondokana na adha ya usafiri, maofisa wa Sumatra watakuwa wanafanya operesheni endelevu kubaini madereva watakaokiuka agizo hilo.

Shiyo alibainisha kuwa tayari utaratibu wa kutumia vibao vinavyoonyesha ruti ambayo mabasi hayo yanatakiwa kwenda vimeanza kutumika ili kuepusha madereva kuiba ruti.

“Pia tumeshawaambia wachore mistari au kuweka stika zenye alama ya rangi za ruti hizo kwa sababu madereva ni wajanja…ikifika usiku wanaweza kutoa kibao na kuiba ruti,”alisema Shiyo.

Amri hiyo imekuja wakati kukiwa na malalamiko kutoka kwa watumiaji wa usafiri wa Uda, wakidai kutozwa gharama kubwa za nauli tofauti na vinavyotozwa na mabasi ya daladala.

Kwa mujibu wa tiketi za sasa za Uda abiria anatakiwa kutozwa kati ya Sh400 hadi 450 kwa umbali wa kilomita 14 na Sh500 hadi 1,100 kwa umbali wa kilomita zaidi ya 20, lakini abiria wamekuwa wakitozwa kinyume na kiwango hicho.

Viwango vya nauli za daladala huanzia Sh400 kwa safari ya umbali wa kilomita 14 hadi Sh750 kwa umbali wa kilomita zaidi ya 20.

Mkurugenzi wa Mafunzo Utafiti na Maendeleo wa Kampuni ya Simon Group inayoendesha shirika hilo, Henry Bantu, alikiri kuwapo kwa mabadiliko hayo ya viwango vya nauli.