Latest Updates

GARI LA RAIS LILILOIBWA KENYA LAPATIKANA UGANDA


Msemaji wa Rais alikana kuwa gari hilo lilikuwa limeibwa

Maafisa wakuu kutoka shirika la polisi wa kimataifa, Interpol amethibitisha kuwa gari la ulinzi wa rais Uhuru Kenyatta lililoibwa mjini Nairobi wiki jana limepatikana nchini Uganda.
Kwa sasa gari hilo limepelekwa mjini Kampala.

Mkurugenzi wa polisi wa kimataifa Interpol nchini Uganda Assab Kasingye aliambia BBC kuwa gari hilo litarudishwa Nairobi.Gari hilo aina ya BMW liliibwa siku ya Jumatano usiku mjini Nairobi. Watu watatu wamekamatwa kuhusiana na wizi huo.
Gari hilo liliibwa na watu waliokuwa wamejihami Jumatano wiki jana.
Hata hivyo msemaji wa serikali Manoah Esipisu alikanusha habari hizo akisema kuwa gari lililoibwa halikuwa na ulinzi wa Rais Kenyatta bali lilikuwa gari kuu kuu la polisi.
Lakini lilikuwa linaendeshwa na afisa wa polisi aliyeripoti kuwa gari hilo ni mmoja ya magari ya ulinzi wa Rais.Afisa huyo wa polisi pia alisemekana kuwa mmoja wa maafisa wa polisi wa ulinzi wa Rais.
Tukio la wizi wa gari hilo, lilisababisha taharuki miongoni mwa maafisa wa ulinzi kwa sababu magari ya ulinzi wa Rais yenyewe yanapaswa kuwa na ulinzi mkali.
Takwimu za polisi zinaonyesha kuwa visa vitatu vya wizi wa magari huripotiwa mjini Nairobi kila siku.
Hiki ni kisa kimoja kati ya vingi vya wizi wa magari ambapo mtu yeyote anaweza kuathirika.