Licha ya mkwanja kumtembelea, msanii wa filamu Bongo, Kajala Masanja amekwama kupata pesa ya kumlipia faini mumewe Faraji Chambo ili aweze kutoka jela.
Akizungumzia ombi la mumewe huyo kumtaka kutofuja pesa badala yake amlipie faini ili aondokane na mateso ya gerezani, Kajala alisema ni kweli anampenda sana mumewe na angetamani kufanya hivyo lakini kiasi cha shilingi milioni 200 kinachotakiwa si kidogo hivyo hawezi kukipata.
“Nampenda sana mume wangu, hilo halina ubishi na pia najua anateseka sana kule gerezani kwani nakujua lakini milioni 200 siyo hela ndogo ujue. “Natamani hata leo niwe nayo nimlipie lakini ndiyo hivyo tena,” alisema Kajala kwa masikitiko.
Hata hivyo, licha ya Kajala kuwa na nia ya kumtoa jela mumewe, mmoja wa mawakili aliyekuwa akihusika na kesi yao aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema:
“Kama Kajala anafikiria kumlipia mumewe faini simshauri afanye hivyo kwani hukumu iliyotolewa ni ya kesi moja na ile nyingine ya kuuza nyumba iliyokuwa imewekwa bondi na Takukuru, bado inaendelea na huwa Faraji anatoka gerezani kwenda mahakamani.
“Sasa Kajala anaweza kutoa pesa zake, mumewe akatoka lakini hukumu ya ile kesi nyingine ikatolewa na akarudi tena jela,” alisema wakili huyo. Hivi karibuni, mume wa Kajala alituma ujumbe kupitia watu wanaokwenda kumtembelea akimtaka mkewe kumuonea huruma na kumlipia faini ili atoke gerezani badala ya kuzitumia pesa kwa anasa.