Latest Updates

SIMULIZI TAMU YA BAHATI BUKUKU


ILIPOISHIA: WIKI iliyopita iliishia pale alipokuwa akijiandaa kufunda ndoa baada ya kuvalishwa pete ya uchumba kanisani huku kila siku alizokuwa akionana na Daniel, ilikuwa ni lazima awe na ndugu zake kwa kuwa naye shetani alikuwa kazini.

ENDELEA..

Mwimbaji wa nyimbo za Injili Bongo, Bahati Bukuku.

Kila kitu kilikuwa kimekamilika, ndoa tu ndiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa. Katika muda wote huo nilikuwa nikionana na Daniel kama kawaida ingawa ilikuwa chini ya uangalizi mkubwa.Siku ziliendelea kukatika na hatimaye baada ya miezi miwili, siku ya ndoa ikapangwa. Moyoni bado sikuwa nikiamini kama kweli na mimi nilikuwa nikienda kuitwa mke wa mtu.

Sikutaka kukaa kimya, kwa sababu kila kitu kilitakiwa kukabidhiwa mikononi mwa Mungu aliye hai, niliendelea kuomba zaidi ili Mungu aweze kufanikisha kila kitu kilichokuwa kikitakiwa kufanyika.
Ashauriwa kuwa mke bora“Kuwa mke bora kama nilivyo,” aliniambia mama, hayo yalikuwa maneno pekee ambayo kila siku alikuwa akiniambia.

“Ninaomba Mungu niwe hivyo,” nilimwambia.
“Sawa. Tutazidi kuliweka jambo hili mbele za Mungu.” Maisha yalisonga mbele huku siku zikiendelea kukatika. Katika maisha yangu hakukuwa na kipindi kigumu na kizuri kama hicho. Sikuwa huru kuongea na mchumba wangu, kila nilipokuwa nikisimama naye kuongea hasa kanisani, kila mtu alikuwa akituangalia.



Mishemishe za ndoa zaanza
Kwa wazazi wangu walivyokuwa na hamu kuona naolewa, siku moja kwao ilionekana kama mwaka mzima. Hawakuficha hisia zao, mara kwa mara walikuwa wakinipigia simu na kuniambia ukweli kwamba walikuwa wakitaka kuiona ndoa yangu kwa hamu kubwa.
“Kuna sare siku hiyo?” aliuliza Neema (rafiki yake).“Zitakuwepo ingawa sijajua zitakuwa za namna gani,” nilimwambia.
Afunga ndoa kanisani
Kwa sababu ndugu zangu hawakutaka kuonekana kawaida, wakaanza kujichangachanga na mwisho wa siku wakaamua rangi ambayo ingependeza sana kuvaliwa siku hiyo, na siku ya ndoa ilipofika, kila mmoja akavaa sare yake kitu kilichowafanya wapendeze sana.

Kanisani, idadi ya watu ilikuwa kubwa. Nilimtumikia Mungu kupitia uimbaji kwa kipindi kirefu hivyo hata kanisani watu walijaa kwa sababu walikuwa wakinifahamu vilivyo na kila mtu alitaka kuishuhudia ndoa yangu.

Siku hiyo itabakia kumbukumbu katika maisha yangu kwani nilifanya tendo ambalo mara nyingi hutokea mara moja katika maisha ya mwanadamu endapo hakutokuwa na kitu chochote kibaya kitakachotokea.
Nilivalia shela langu huku Daniel akiwa ndani ya suti, baada ya hapo, mchungaji akafungisha ndoa na hatimaye kuanza kuishi kama mume na mke.



Aendelea kumuimbia Mungu
Maisha yangu ya uimbaji hayakufikia mwisho, japokuwa nilikuwa mke wa mtu lakini mara kwa mara nilikuwa nikiimba huku moyoni mwangu nikiwa na lengo la kuwa mtu mwenye uwezo mkubwa kifedha ambao utaweza kunisaidia katika maisha yangu, mume nwangu na watoto wangu.

Kama unakumbuka, nilizaliwa mkoani Mbeya, nyumbani hatukuwa matajiri, tulikuwa watu wa kawaida sana na kama ungetusimamisha mbele ya watu wengine, basi tungeweza kuonekana mafukara.



Ayapanga maisha ya watoto wake
Maisha niliyopitia kipindi cha nyuma, tabu nilizozipata sikutaka wazipate watoto wangu hivyo nilijiona kuwa na jukumu kubwa la kutaka kuyatengeneza maisha ya watoto wangu hapo baadaye.
“Nitakuwa na fedha sana, sipendi kuona watoto wangu wakiteseka, nataka kila mmoja awe na maisha mazuri, wapate wakitakacho,” nilijisemea kila nilipokuwa nikiandika wimbo.

Baada ya kipindi fulani kupita nikaamua kwa moyo mmoja kwamba nilitakiwa kuwa na albamu ya nyimbo zangu. Kama kuimba makanisani niliimba sana na katika kipindi hicho nilitakiwa kuwa na hazina ya kazi zangu ili zisiweze kusahaulika masikioni mwa watu.



Atoa albamu
Mpaka kufikia hatua hiyo, tayari nilikuwa nimepitia mapito kadhaa mpaka kufikia hatua hiyo hali iliyosababisha kuiita albamu hiyo jina la Yashinde Mapito.
Ilikuwa ni albamu nzuri iliyosheheni nyimbo zilizowagusa watu wengi hasa wenye safari ndefu ya kuelekea mbinguni.

Kupitia albamu hiyo, nikauona mkono wa Mungu kwani nilifanikiwa kwa kiasi kikubwa na kufanya mambo mengi katika maisha yangu.Ashauriwa kutokumuacha Mungu
Kufuatia mafanikio niliyopata na mama kusikiliza nyimbo zangu, nilimwambia kulikuwa na mambo mengi ya kufanya.

“Najua, ila kumbuka usimuache Mungu, kuna mengi atakufanyia katika maisha yako,” mama aliniambia.
Siku hiyo niliongea naye mengi kuhusu albamu yangu na maisha yangu kwa jumla. Kama jina la albamu yangu ilivyokuwa ndivyo ambavyo nilivyokuwa nikipitia katika maisha yangu.



Mapito yenyewe
Maisha yangu yalijaa mapito ya kila namna, nisingependa kuyataja kwa sababu yamekaa kibinafsi zaidi.
Sikutaka kuwasikiliza watu, kitu pekee nilichokuwa nikikifanya ni kupiga magoti na kuanza kuomba huku nikisaidiwa na mume wangu ambaye kila siku alinitia moyo.

Maneno mengi yalikuwa yakizungumzwa kwa watu kuhusiana na maisha yangu lakini yote hayo niliyapuuzia na kuona kwamba ni shetani ndiye alileta vyote hivyo ili nianguke dhambini na kuanza kumtumikia.

Nilimuuliza mume wangu kwamba majaribu niliyopata yangeisha lini?
“Yatakwisha tu, cha msingi tumuombe Mungu.”
Siku zote maishani mwangu zilikuwa ni siku za kumuomba Mungu tu, sikuchoka na wala sikukoma kwani niliamini kwamba Mungu yuleyule nikimuabudu tangu utotoni ndiye angenitangulia na kunilinda mpaka muda huo.

Pamoja na albamu kuuza sana, lakini waliibuka watu ambao walifanya juu chini kunipoteza na hata kutaka kufanya utapeli wa fedha ambazo zilipatikana katika mauzo ya albamu hiyo ila nilimshukuru Mungu kwa kuwa walishindwa na kuendelea na maisha yangu.

“Mungu ni muweza, utashinda tu hivi vita, fedha zako zitakuwa zako milele,” aliniambia baba.
Baba aliponitia moyo kwa maneno hayo, nilimweleza kuwa kwa kuwa nilimuomba Mungu kila siku angenipigania.

“Omba sana,” baba aliniambia.
Nilimwambia nao walitakiwa kuniombea.
“Hakuna tatizo, roho ya utapeli imeshindwa kwa jina la Yesu,” baba aliniambia.
Baba aliponieleza hivyo nilisema, ameni.
Je, nini kiliendelea? Tukutane Alhamisi ijayo!

- See more at: http://mdadisihuru.blogspot.com/2014/09/simulizi-tamu-ya-bahati-bukuku.html#sthash.opabfwdO.dpuf