AUAWA KWA KIPIGO BAADA YA KUIBA MADIRISHA KAHAMA
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Ramadhan Majaliwa mkazi wa Majengo mjini Kahama mkoani Shinyanga ambaye ni fundi nyumba amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Kahama baada ya kupigwa na kisha kuchomwa moto na wananchi kwa tuhuma za kuiba madirisha ya nondo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Noel Mseven tukio hilo limetokea leo majira ya saa 11 alfajiri ambapo mtuhumiwa alivunja madirisha hayo katika nyumba inayoendelea kujengwa na baadhi ya watu kumuona.
Amesema wanachi walianza kumfuatilia na walipomkamata alianza kukimbia ndipo wananchi hao wakapiga kelele na kusababisha kumkamata na kuanza kumrushia mawe kisha kumchoma moto kwa mafuta ya Petroli ambayo yalipatikana katika pikipiki.
Mseveni amesema mtuhumiwa huyo alijirusha kwenye mtaro wa maji na moto huo ukazima na kwamba ilipigwa simu kwa jeshi la polisi ambao walifika eneo la tukio na kumpeleka katika hospitali ya wilaya ya Kahama.
Akiongea kwa shida katika hospitali ya hiyo kabla ya kifo chake mtuhumiwa huyo alisema alipigiwa simu na dada mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Manka kwamba afuate mzigo huo ili ampelekee na ghafla wananchi walimzingira na kuanza kumpiga na kumchoma moto.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana zinasema kuwa Majaliwa alifariki dunia muda mchache badae wakati akipatiwa matibabu hospitalini hapo kutokana na kuungua vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake.
Hata hivyo mmiliki wa Nyumba iliyobomolewa madirisha hayo bado hajajulikana kutokana na kuwa bado inaendelea kujengwa.
Jeshi la polisi wilayani Kahama limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na linaendelea na uchunguzi zaidi.
Posted