HUYU NDIYO CHEGE,SOMA HAPA UFAHAMU USIYO YAFAHAMU KUHUSU CHEGE
Said Nassoro ‘Chege Chigunda’.
NAPOTAJA makundi yanayofanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva bila kupepesa ni lazima utalitaja Kundi la TMK Wanaume Family. Ndani yake kuna vichwa vingi ambavyo vinaunda kundi hilo na kati yao ni Aman James ‘Mheshimiwa Temba’ na Said Nassoro ‘Chege Chigunda’.
Vijana hawa wamefanya mabadiliko makubwa katika muziki ndani na hata nje ya kundi. Kuna kazi za pamoja ambazo wameimba kama vile Tunafurahi na nyingine nyingi. Kuna wakati utawasikia wakitoa wimbo kwa pamoja na wakati mwingine utamsikia mmoja-mmoja (solo).
Wakati huu, Chege ameachia wimbo wa Chapa Nyingine ambao ni miongoni mwa nyimbo ambazo zinafanya vizuri sana kwa sasa katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni.
Ukiachana na Chapa Nyingine tayari ameshawahi kufanya nyimbo nyingine kali ambazo zilitikisa Bongo kama Take Away remix ambayo aliimshirikisha Diamond Platinumz.
Katika makala hii Chege anafunguka zaidi juu ya wimbo huo na maisha yake kimuziki kwa ujumla:
Nini maana ya Chapa Nyingine?
Chapa Nyingine ni wimbo ambao umetokana na shoo tulizokuwa tukipiga tukiwa jukwaani. Ilikuwa kila tukitaka tupigiwe biti na Dj tunamwambia Chapa Nyingine na yeye anapiga nyingine tena na tuliposhuka jukwaani mashabiki wakaupenda sana msemo wa Chapa Nyingine, ikatubidi tupange na kuona ni ‘idea’ nzuri tunaweza kuifanyia kitu, ‘then’ tukaifanyia kazi na imekuwa kama unavyoiona na kuisikia.
Yule ambaye nimemshirikisha ni mwanamuziki mpya na ni mdogo wangu wa mtaani anaitwa Gift nilimsikia akiimba vizuri nikaamua nimshirikishe kwenye huu wimbo.
Vipi kuhusu kufanya kolabo nyingine na Diamond?
Nafikiri tumeshafanya na imeshatoka ambayo ni Uswazi Take Away Remix. Ikitokea nafasi nitafanya naye kazi nyingine lakini kwa sasa nipo natengeneza wimbo mpya na Temba na utatoka hivi karibuni.
Game ya sasa unaionaje?
Inaelekea pazuri kwa sababu ushindani kwa sasa ni mkubwa sana na muziki umekuwa ukitutengenezea pesa vizuri kila siku, ninachokiomba kwa serikali kama ikituchekia vizuri suala hili itakuwa ni ajira ya kudumu.
Kitu gani unakipenda katika muziki?
Kikubwa zaidi ninachokipenda ni pale unapotoa kazi na kupokelewa vizuri na mashabiki, hilo ni jambo kubwa sana la kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Maisha ya kimuziki unayaonaje?
Ni magumu kwa kweli! Tofauti yake ni kwamba unapokuwa mtu maarufu matatizo yanakuwa mengi yaani huwezi kuwa huru, unakuwa mtu wa kukaa sehemu za kuchagua na mbaya zaidi huwezi kupanda hata daladala.
Malengo yako katika muziki ni yapi?
Kikubwa kwa sasa ni kufika mbali sana. Nimekuwa nikijitahidi kila kukicha kuhakikisha nafanya vizuri katika muziki kwa kutoa nyimbo zangu sambamba na video zenye ubora wa hali ya juu ili mashabiki wangu wafurahie na kwa hilo nadhani ninapoelekea kwa sasa ni pazuri.
Vipi kuhusu kufanya kolabo nje ya nchi?
Unajua hiyo huwa inatokea tu mtu kufanya kolabo na mwanamuziki wa nje ya nchi, kwa upande wangu bado sijaipanga akilini mwangu, kwani naamini chochote kinaweza kufanyika bila hata ya kufanya kolabo na mtu yeyote wa nje ya nchi na ukakubalika kimataifa zaidi
Posted