Latest Updates

MILLEN MAGESE: WATU WAREFU NA WEUSI TUNANYANYASIKA VIWANJA VYA NDEGE


Kukamatwa kwa baadhi ya watanzania katika nchi mbalimbali wakihusishwa na ubebaji wa dawa za kulevya kumeathiri idadi kubwa ya wasafiri wanaotumia hati ya kusafiria ya Tanzania kutokana na kukaguliwa kupita kiasi....


Mmoja wa waathirika wa ukaguzi huo ni Miss Tanzania wa mwaka 2001, Happines ( Millen ) Magese ambaye alisema kukamatwa kwa watanzania hao wanaotuhumiwa kuhusika na ubebaji wa dawa za kulevya umetia doa watanzania wanaosafiri nje ya nchi kwa kutumia hati hiyo...


"Wakati nikitumia pasipoti ya Tanzania huwa napekuliwa kupita kiasi, hasa kutokana na urefu wangu na kuwa na Passport ya Tanzania na pia ni mweusi," anasema Millen


Mrembo huyo anayefanyakazi katika nchi mbalimbali ikiwemo Canada na Marekani, kwa sasa anaishi katika jiji la New York nchini Marekani na anatoka katika familia ya watoto watano,wasichana watatu na wavulana wawili.


Akisimulia kuhusiana na utata wa jina lake la Happines na kuwa Millen, mrembo huyo aliyeshawishiwa kuingia katika mashindano ya urembo na mrembo mwenzake aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2000,Jacqueline Ntuyabaliwe ( K-Lynn), alisema jina hilo lilitokana na mapendekezo ya mkurugenzi wake aliyetaka jina lake lingine la kipekee tofauti na jina la Happiness.


"Unajua jina hili lilitokea siku ya pili tu nilipofika Afrika Kusini, ambapo mkurugenzi wa kampuni ya urembo ya Ice Models, Jane Celliers ambaye sasa ni meneja wangu alitaka nimtajie majina yangu mengine, nikamtajia majina yangu ya Mwanza ambayo ni Ngaile na Millen, pia nikamtajia majina yangu ya Tanga ambayo ni Baina na Lilian pamoja na jina langu la ubatizo la Happiness yeye akachagua jina la Millen akadai lipo kipee ndio maana nalitumia kimataifa"