Swali kwa Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa
Kaka Ben nakusalimu!
Mtani wangu na kada mwenzangu chamani,pia Mwenyekiti wangu na Rais wangu wa zamani,natumai uko salama. Pole kwa mihangaiko na purukushani za kimaisha na za kikampeni. Kwanza nikupe habari kuwa mimi Mzee Tupatupa toka mkoani Ruvuma nimejiondoa kwenye timu ndogo ya kamepeni za Dr. Magufuli. Wewe na wenzako,na aina mpya yenu ya siasa za kejeli na 'mipasho' mmeniondoa kampenini.
Leo,sikuja kuchambua kilichosemwa Jangwani siku ya Jumamosi kwa ujumla wake. Nimekuandikia kukuuliza swali moja tu mtani wangu na kaka yangu Ben. Umesema kuwa chama au vyama vinavyojiita ni vya ukombozi, wakati ukombozi wa Tanzania ulishapatikana, ni wapumbavu na malofa. Ukasema kuwa ukombozi ulipatikana kwa harakati za TANU na ASP ambazo zimezaa CCM. Nimekuelewa kivyangu.
Sasa, kaka Ben, chama kinachojiita CHAMA CHA MAPINDUZI, wakati mapinduzi yalishafanyika huko Zanzibar mwaka 1964 na kwasasa hakuna mapinduzi mengine kinaitwaje na waliomo humo waitwaje? Tafadhali tuchagulie jina sisi wanachama na wafuasi wa chama cha mapinduzi ambayo kwasasa hayapo tena!
Posted