Mazishi
ya Mzee Madiba aliyefariki dunia Desemba 5, 2013 yalifanyika katika
kijiji alichokulia, Qunu, Mkoa wa Mthatha katika Jimbo la Eastern Cape
nchini humo.
Wiki iliyopita, serikali ya Afrika Kusini ilitoa amri kwamba
haruhusiwi mtu yeyote kupiga picha ya mwili wa marehemu akiwa anaagwa
jijini Pretoria.
Familia nayo ikapigilia msumari wa mwisho ikisisitiza kuwa, binadamu
yeyote mwenye akili timamu haruhusiwi kupiga picha ya mwili huo ukiwa
ndani ya jeneza.
Amri hiyo ilivivunja nguvu vyombo mbalimbali vya habari duniani
ambavyo vilikuwa nchini humo vikifuatilia mazishi na maziko ya Mandela.
Serikali iliweka wazi kwamba, mtu yeyote atakayepiga picha, akinaswa
zitafutwa kwanza halafu kama ni Msauzi atashitakiwa na kama ni raia wa
nje atarudishwa nchini mwake na kupigwa marufuku kuingia nchini humo
maishani mwake.
Baadhi ya watu nchini humo wamekuwa wakihaha kupata picha hiyo ili waitengenezee fremu na kuiingiza sokoni kwa wanunuzi.
Juzi, baadhi ya mitandao iliweka sehemu ya sura ya Mandela na kudai ni picha yake akiwa kwenye jeneza siku chache baada ya kifo.
Hata hivyo, haraka sana, baadhi ya vyombo vya usalama nchini humo
vilikanusha na kusema picha hiyo ni enzi za uhai wake akiwa amelala.
Ukawekwa ushahidi wa picha hiyo ikiwa yote ambapo Mzee Madiba alikuwa akiuchapa usingizi wakati fulani enzi za uhai wake.
Kuhusu
maziko yake, zaidi ya wageni 4,500 kutoka pande zote za dunia
walihudhuria ndani ya hema kubwa lililojengwa katika eneo la familia ya
Mandela huku mamia ya wanakijiji na baadhi ya wanafamilia wakikosa
nafasi ya kuuaga mwili wa mpendwa wao huyo.
Idadi kubwa ya viongozi waliohudhuria, wakiwemo Rais Barak Obama wa
Marekani na mtoto mkubwa wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles,
kumelifanya eneo la kijiji hicho kuwa dogo na linalohitaji uangalizi wa
hali ya juu wa usalama. Katika kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa
kiusalama, ndege mbili za jeshi la nchi hiyo zilikuwa angani pamoja na
helikopta kadhaa.
Zaidi ya wanajeshi 20,000 walilinda usalama katika kijiji hicho wakifanya kazi sambamba na jeshi la polisi.
Licha
ya wenyeji na majirani hao wa marehemu Mandela kunyimwa fursa ya kuuaga
mwili huo, pia walizuiwa kuukaribia kutokana na uhaba wa nafasi,
kitendo ambacho kililalamikiwa sana.
Waliokosa nafasi ya kuhudhuria mazishi hayo siyo tu majirani, bali
hata mtoto wa kaka mkubwa wa Mandela, Maurice aitwaye Mzwandile Mandela
mwenye umri wa miaka 13.
Mwingine ni mpwa wa Mandela, Gloria Mkwedini, mtoto wa dada yake
ambaye pia hakuhudhuria mazishi hayo pamoja na familia yake ya watu 16.
Watu
hao wanaishi maili chache kutoka kwa Madiba wakiwa wanaishi katika moja
ya nyumba nyingi za mduara zilizoko katika eneo hilo.
Na kwa vile hakuna umeme, hawakuweza kufuatilia tukio hilo katika televisheni.
‘Hii
imetufanya tujione kama ni watu wageni tuliotengwa,” alisema Gloria
akimlaumu mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, Makaziwe, 59, aliyedai kuwa
ndiye aliyekuwa anaamua nani aalikwe na nani aachwe.
Alisema mume wake alimfuata Makaziwe na kutaka kupewa mwaliko, lakini
binti huyo alikataa. Alilalamika kuwa kunyimwa kwao mwaliko kunatokana
na umasikini wao.
Mandela alizikwa kimila, kwa ndugu wa karibu wa familia yake pamoja
na viongozi wa kimila wapatao 70 waliokabidhiwa mwili huo na kuuingiza
ndani ya nyumba yake ya milele huku pia wakikataa tukio hilo kurushwa na
chombo chochote cha habari.
Miongoni mwa mila na desturi za kabila la Mandela linalofahamika kwa
jina la Aba Thembu ni pamoja na kuchinjwa kwa ng’ombe dume aliyenona na
damu yake kumwagiwa ndani ya kaburi la marehemu.
Taifa la Afrika Kusini limekuwa lenye pilikapilika nyingi tangu
kufariki dunia kwa mpigania haki huyo Desemba 5, mwaka huu, nyumbani
kwake jijini Johannesburg baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa
mapafu.
Mwili wake uliondolewa saa tisa usiku na kupelekwa katika hospitali
ya kijeshi jijini Pretoria ambako kwa siku tatu kuanzia Jumatano,
uliwekwa katika majengo ya Ikulu ambako zaidi ya watu laki moja
waliripotiwa kuuaga.
Hata hivyo, serikali ilitoa amri ya kusitishwa kwa shughuli hiyo huku
maelfu ya wananchi wakiwa katika msururu mrefu wakisubiri kupata nafasi
ya kumuaga mtu anayedhaniwa kuwa ndiye maarufu na mwenye heshima zaidi
kuliko wote katika karne ya 21.