Latest Updates

DARASA NDO HILI>>>MKITOKA UGOMVINI, KUWA MWANGALIFU KUSAMEHE




KUNA mambo mengi yanatokea katika hii dunia, ambayo wakati mwingine yanatulazimisha kuzungumza na watu wetu ili kuwapa kile kidogo tunachokijua, tukiamini mchango wa mawazo yetu unaweza angalau kuongeza wigo wa ufahamu juu ya kitu kinachosababishwa na mapenzi.

Kupitia vyombo vya habari, yakiwemo magazeti redio na televisheni, tutakuwa tunaona na kusikia kuhusu wapendwa wetu wanavyopoteza maisha kutokana na mapenzi. Juzi, nilikuwa napitia habari moja hivi kutoka Tarime kule Mara, ikaniuma sana. Mdada mmoja alipigwa na mumewe na kupewa majeraha makubwa sana, eti tu kwa sababu alichelewa kupata ujauzito.

Lakini kama kuna tukio liliniharibia siku katika mwezi huu wa kwanza wa mwaka, basi ni ile ishu ya jamaa aliyemchinja mkewe pale hotelini Manzese jijini Dar es Salaam. Ninajaribu kulizungumzia suala hili ili likusaidie katika maisha yako ya kimapenzi kwa sababu ninaliona ni tukio linalojirudia kati ya wapenzi wa kada mbalimbali.

Jamaa alikuwa hana maelewano mazuri na mke wake, wakiishi kwa migogoro isiyokwisha, kiasi kwamba mwanamke akaamua kuondoka nyumbani kwao na kwenda kwa kaka yake, angalau akapumzike kwa muda. Ni vigumu kidogo kujua chanzo cha ugomvi wao, lakini tunaelezwa kuwa baada ya mama kuondoka, baba alimfuata na kumtaka wasahau tofauti zao, warejee katika uhusiano wao kama zamani.

Kinachoonekana ni kwamba mume hakuwa na dhamira ya kusamehe, kwani baada ya mwenzake kumwelewa vizuri, akakubali kuandamana hotelini ambako walikubaliana wakakae na kuzungumza yao. Matokeo yake, akatumia kisu alichokuwa nacho na kumuua mwenzake kikatili.

Orodha ya watu wanaopoteza maisha kwa sababu ya wivu wa mapenzi ni ndefu sana na kila wahusika, wana simulizi tofauti na mwingine ingawa zote ni za aina moja. Nataka nizungumzie hili la kugombana, mkafikia sehemu ya kununiana, kuhama nyumba au chumba na baadaye kurejeana.

Kwanza kabisa ieleweke kuwa ugomvi baina ya wanandoa au walio katika uhusiano ni jambo la kawaida kabisa. Sitaki kujiongopea au kukupa nafasi ya kuwaongopea wengine kuwa hili ni jambo jipya. Kila siku, sehemu fulani kuna wanandoa wanazozana, wanapigana, wanatengana na kadhalika. Tatizo linalotutofautisha kati yetu sisi na wao ni namna tunavyoumaliza ugomvi wetu.

Kuna watu hawamalizi wiki bila kuzozana ndani ya nyumba yao, lakini wakiwa nje, hakuna mtu anayefahamu kilichotokea. Unaweza kuwa shahidi kuwa umeshawahi kusikia mara nyingi juu ya ugomvi wa watu ambao siku zote uliamini wanapendana sana.

Ugomvi unaomalizika kwa mmoja kuondoka ndani ya nyumba, ni wazi kwamba umefikia kiwango ambacho hakivumiliki. Mtu anaona ni bora aondoke kidogo ili kupoza hasira iliyopo, kutuliza hali ya hewa au kutoa nafasi kwa watu zaidi kushiriki katika kutafuta suluhisho la ugomvi huo.

Sasa katika ugomvi kama huo, mambo mengi yanakuwa yamefanyika baina ya wanandoa. Kitendo cha kuondoka nyumbani kinaleta tafsiri tofauti kwa anayebaki, wengi wanafikiri kuhusu kutolewa kwa siri zao nje. Huamini kwamba huko walikoenda, wanazungumza kuhusu udhaifu wao, kitu ambacho wengi hawapendi.
Ninachotaka kusisitiza ni kwamba sisi tunajua tunapogombana, nani anakuwa amekosea na nini suluhisho lake. Tunajua kwa namna gani mwenza wetu ameumia au amekwazwa.

Jambo la muhimu
tusimuamini mara moja, mtu ambaye siku chache nyuma, alitishia kutoa uhai wetu anapokuja kuomba tumalize tofauti zetu kirahisi.